RC Manyara ajikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa

 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo.
 
 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo, amejikuta katika wakati mgumu baada ya wananchi wa wilaya ya Kiteto,  kumzomea na kumtaka aondoke na mkurugenzi wake wakati alipokutana nao kuzungumzia  mgogoro wa wakulima na wafugaji.

Hali hiyo ilijitokeza wakati mkulima,  Ramadhani Machaku, aliposimama kuuliza swali, lakini Mkurugenzi wa Wilaya ya Kiteto, Jane Mutagurwa, kumnyang’anya kipaza sauti na kumtaka aulize swali badala ya kutoa hotuba.


Katika swali lake Machaku, alishutumu uongozi wa wilaya kuwa umechangisha mamilioni ya fedha kwa wafugaji ili kuhakikisha wakulima wanaondoka na matokeo yake kule mashambani wanaishi kama maadui na kuuana kinyama.


Aidha alisema kuwa viongozi wamekuwa hawataki kuongea ukweli kuhusu jambo hilo na kudai kuwa hawataondoka katika eneo hilo hadi hapo serikali itakapowahakiki wafugaji ambao ndiyo waliowauzia maeneo.


Alimuomba Rais Jakaya Kikwete au Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati kutatua mgogoro huo kutokana na viongozi wa wilaya hiyo kuwagawa wananchi na kupindisha ukweli.


Hatua ya mkurugenzi huyo kumnyang’anya kipaza sauti, kiliwakasirisha wananchi hao, ambao walianza kuzomea  huku baadhi wakisusia na kuanza kuondoka  kwenye mkutano huo, wakitaka Mkuu wa mkoa aondoke na mkurugenzi wake.


Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kiteto, Foka Dinya, aliingilia kati na kuwataka wananchi hao kuacha vurugu.


 Awali  Mbwilo ambaye alitoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali, alikiri kuwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto unasababishwa na viongozi wa wilaya hiyo na kuiagiza kamati ya ulinzi ya mkoa kukaa kuangalia tatizo ili wilaya hiyo iwe na amani.


“Mambo haya tangu mwanzo nayafahamu lakini bado tunayafanyia kazi lakini ni kwa nini watu wanakubali kuchangishwa fedha bila ya utaratibu wa serikali na bila kibali maalum sisi kama serikali tunalifuatilia haiwezekani michango ichangishwe kikabila,”alisema.


Alisema kuwa  serikali ya mkoa inatambua suala hilo la viongozi kuhusika na mgogoro huo.


Alisema kuwa tangu juzi amefanya ziara na kupokea malalamiko na taarifa kuwa viongozi wa wilaya walipokea rushwa ya madume ya ng’ombe kutoka kwa wafugaji ili wakulima waondolewe katika Hifadhi hiyo.


“Wananchi kweli mmegawanywa katika makundi na inawezekana ni sisi viongozi ndiyo tuliofanya hivi na matokeo yake wafugaji wanaona wana haki ya kukaa ndani ya hifadhi huku wakulima nao wanaona wamehujumiwa kwanini wafugaji wakubaliwe,” alisema Mbwilo.


Alisema kuwa mgogoro huo ulitokana na baadhi ya wakulima kuingia katika eneo la hifadhi kinyume na sheria na kujichukulia ardhi kubwa mpaka kumiliki hekari 6000.


Aliwataka wakulima na wafugaji kuondoka katika hifadhi hiyo mpaka hapo watakapofanya utaratibu wa kugawa tena kulingana na vielelezo  watakavyowasilisha kuwa walipewa idhini na nani ya kumiliki maeneo hayo.


Aliwaagiza viongozi wa wilaya kuwaondoa katika eneo hilo wakulima na wafugaji wote kwa pamoja kwa kuwa wameingia kinyume na sheria tofauti na agizo la awali ambalo liliwataka wakulima kuondoka.


Awali mmoja wa wafugaji wa jamii ya Kimasai, Kisioki Masiyai, alisema kuwa chanzo cha mgogoro na kusababisha mapigano ni Mkurugenzi wa wilaya hiyo, ambaye aliwachangisha fedha wafugaji ili kuwaondoa wakulima.



Alisema kuwa hawatakubali kuondoka katika hifadhi hiyo mpaka hapo serikali ya wilaya hiyo itakapotoa mchanganuo wa matumizi ya mamilioni ya fedha ambazo walichangishwa wafugaji.
 

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Jambo Tz