MTOTO wa kaka wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu
na Bunge, Willium Lukuvi, aitwaye Tomm Malenga, ambaye ni katibu wake,
amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kukamatwa kwa
tuhuma za kuhusishwa na ujangili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, Willium Lukuvi.
Habari zilizopatikana mjini hapa, juzi Jumapili, Oktoba 27, mwaka
huu, zinasema akiwa ofisini kwake siku hiyo, Tomm alifuatwa na maofisa
wa Wanyama Pori kwa kile kilichotajwa kuwa anahusika na ujangili.“Walifika na kumkamata kisha wakaanza kumpiga, tena palepale ofisini kwa Lukuvi. Amevunjika vidole vya mguu na mkono wake mmoja hauko sawa baada ya kipigo hicho,” alisema mtoa habari wetu.
Tomm hakupatikana ili kuzungumzia sakata hilo lakini waziri Lukuvi alifafanua baada ya kuzungumza na mwandishi wetu ambapo alisema kilichofanyika anakijua na kwamba ni njama za wabaya wake.
“Sikiliza bwana, licha ya Tomm kuwa msaidizi wangu wa jimboni ni mtoto wa marehemu kaka yangu. Wanasema eti ametajwa kwenye ujangili; sasa kutajwa tu, unawezaje kwenda kumchukua mtu ofisini kwake, tena kwa kumpiga? Huo siyo utawala wa kisheria,” alisema waziri Lukuvi.
Alisema, mtu aliyemtaja Tomm ni Gedi ambaye alikuwa wa kwanza kukamatwa kwa ujangili na akasema amekuwa akishirikiana na mwanaye.
“Ukweli ni kwamba huyo Gedi ana usongo na mimi, kwani huwa ananipinga tangu mwaka 1995. Aliwahi kugombea udiwani, tukagundua kuwa ni Msomali, tukamfuta. Nadhani anatumia mwaya huo kunichafu mimi na familia yangu,” alisema Lukuvi.
0 comments:
Post a Comment