HAWA NDIO WANAWAKE WAUZA MADAWA YA KULEVYA MATAJIRI NA WAKONGWE DUNIANI

IPO  dhana kwamba wanawake ni daraja hatari sana. Machoni huonekana laini lakini wanaweza kutenda mambo ambayo ni vigumu kwa mtu wa jinsia ya kiume. Biashara ya madawa ya kulevya inahitaji watu hatari, katili, wenye roho isiyotishika.
Mireya Moreno Carreon.
Nancy Botwin katika ‘siriz’ yake ya Weeds kwenye TV, anajaribu kuonesha jinsi mwanamke anaweza kuwa hatari katika biashara ya bangi na madawa ya kulevya kwa jumla, hata hivyo katika uhalisia, hajawafikia hata chembe wanawake hawa hatari ambao wameitikisa dunia.
Hawa ni maharamia 10 wauza unga, wametengeneza fedha nyingi na kila mmoja ameshahusika kwa namna moja au nyingine na mauji. Kwa muuza madawa ya kulevya, kitendo cha kutoa roho ya mtu kipo jirani yake sana.

1. GRISELDA BLANCO

Inawezekana huyu ndiye akawa muuza unga mwanamke katili, mwenye uwezo mkubwa kuliko wote kuwahi kutokea katika historia ya dunia. Ameshahusika na mauaji ya watu zaidi ya 200. Ni raia wa Colombia, akiwa na miaka 11, tayari alishahusika na tukio la utekaji wa mtoto. Baadaye alihamia Marekani, kwenye Jimbo la Florida ambako alitengeneza mtandao wa madawa ya kulevya ambao ulimpa utajiri mkubwa.

2.  SANDRA AVILA BELTRAN

Ni raia wa Mexico, alizaliwa mwaka 1960. Aliwahi kupewa jina la Mungu wa Kike wa Madawa ya Kulevya. Vyombo vya habari nchini mwake vikamwita Malkia wa Pacific. Serikali za Marekani na Mexico zinamtaja kuwa kiungo wa magenge ya unga ya Sinaloa Cartel la Mexico na Norte del Valle Cartel la Colombia. Anadaiwa kujipatia mabilioni ya dola kwa usafirishaji wa unga kati ya Colombia, Mexico na Marekani. Kwa sasa yupo gerezani nchini Mexico kwa kosa la utakatishaji wa fedha haramu.

3. ANGIE SANCLEMENTE VALENCIA

Ni raia wa Colombia, aliwahi kushika taji la urembo la taifa katika nchi hiyo lakini alinyang’anywa baada ya kubaini ameshaolewa. Mume wake alikuwa mmoja wa vinara wa unga na walipoachana, alitumia njia zilezile kujipatia utajiri haramu. Alikuwa na genge kubwa la wasafirishaji wa cocaine na kila mtu alimlipa dola 5,000 kwa safari moja. Alisafirisha zaidi Argentina, Uingereza na Mexico. Ana umri wa miaka 35, yupo gerezani Argentina tangu Oktoba 27, 2010.

4. KATH PETTINGILL

Alizaliwa mwaka 1935. Jina lake la utani ni Bibi Kizee Shetani (Granny Evil). Ni mwenyeji wa Jiji la Melbourne, Australia. Alianza kama kahaba kabla ya kugeukia madawa ya kulevya. Alipoteza jicho moja baada ya kupigwa risasi katika moja ya matukio ya uharamia, akimtetea binti yake, Vicky, aliyekuwa anadaiwa dola 300 na maharamia wenzake. Nguvu ya mtandao wa unga aliyoitengeneza, ni hatari na imehusika na mauaji mengi nchini Australia.

5. ENEDINA ARELLANO FELIX

Katika genge ambalo lilikuwa linaongozwa na kaka zake, Ramon na Eduardo, mwanzoni yeye alishika nafasi ya umeneja wa fedha. Baada ya Ramon kuuawa na Eduardo kukamatwa, alishika uongozi. Maofisa usalama wa Mexico waliwahi kukiri kwamba Enedina ndiye alikuwa dira ya kaka zake. Ana umri wa miaka 52, ni msomi mwenye shahada ya uhasibu. Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo. Amebadili mfumo na sasa anaendesha kazi zake kisayansi,
hakuna fujo za magenge ya wahuni kiasi kwamba inakuwa ngumu kumtia hatiani.

6.  BLANCA CAZARES SALAZAR

Ni raia wa Mexico, alianza kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu, aliponogewa akajikita kwenye unga. Ana umri wa miaka 37. Biashara yake ameitanua na yupo makini sana. Anaongoza mtandao mkubwa wenye makundi 42. Ni ngumu kumkamata kwa sababu hahusiki moja kwa moja. Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo.
7. MARIA JIMENEZ

Ana umri wa miaka 27. Alikuwa kiongozi wa genge lililokufa la La Tosca. Baada ya kufanya biashara kwa muda mrefu, alikamatwa mwaka jana nchini kwake Mexico kwa tuhuma za usafirishaji wa unga na mauaji. Baadaye alikiri kuua watu 20 na mpaka sasa yupo jela.

8.  EDITH LOPEZ LOPEZ

Anajulikana kama Malkia wa Kusini. Amekuwa kinara wa madawa ya kulevya tangu alipoolewa na haramia wa unga, Raul Nunez Morales, maarufu kama The Cowboy. Tangu mwaka 2000, Edith amebaki kuwa mmoja kati ya wanawake tisho kwa biashara hiyo haramu duniani.
9. THELMA WRIGHT

Alishirikiana na marehemu mumewe, Jackie Wright katika biashara ya unga kati ya miaka ya 1980 na 1990. Mwaka 1986, mumewe aliuawa, kwa hiyo akashika usukani kwa kulisuka genge lao la Black Mafia ambalo lilifanya matukio mengi. Hata hivyo, kwa kuhofia maisha ya mtoto wake, Jackiem,  kuharibika, aliachana na kazi hiyo na kufanya shughuli nyingine halali. Ni mara chache sana kutokea.

10. MIREYA MORENO CARREON

Ndiye mwanamke pekee kushika nafasi ya juu kwenye Genge la Zetas. Ndani ya kipindi kifupi alifanya matukio mengi ya utakatishaji wa fedha haramu na usafirishaji wa unga. Akiwa nchini kwake, Mexico, mwaka 2010, maofisa usalama wa siri walimkamata akiwa akiwa na gari lenye cocaine na bangi na mpaka leo yupo korokoroni.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by Jambo Tz