Wananchi wa Kenya wameshangazwa na taarifa ya
mwanamume mmoja aliyedhaniwa kuwa mfu kufufuka kutoka katika chumba cha
kuhifadhia maiti katika hospitali moja mjini Naivasha umbali wa kilomita
tisini kutoka mji mkuu Nairobi.
Mwanamume huyo Paul Mburu mwenye umri wa miaka 24, alipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kunywa sumu kwa lengo la kujitoa uhai,kutokana na ugomvi wa kinyumbani na babake ingawa alisemekana kufariki Jumatano usiku wakati akipokea matibabu.
Afisaa mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo ya wilaya, Dokta Joseph Mburu, alisema kuwa dawa iliyotumiwa kumtibu Mburu hufanya moyo kupiga polepole hali ambayo huenda ilimfanya muuguzi kudhani kuwa mgonjwa alikua amefariki.
Mwanamume huyo alisikika akimtaka mmoja wa wafanyakazi katika chumba cha kuhifadhia maiti kumsaidia kwani alikuwa anahisi baridi kali na hapo ndipo mmoja wa wafanyakazi alipotimua mbio kwa hofu.
Nusura Mburu awekwe kwenye jokovu la kuhifadhia maiti.
Jamaa za mwanamume huyo akiwemo babake walikuwa wametembelea chumba cha maiti siku ya Alhamisi ili kujiandaa kwa mazishi , lakini baadaye mchana walifahamishwa kuwa Mburu alikuwa hai.
0 comments:
Post a Comment