Mbunge wa jimbo la Ubungo (CHADEMA) Mh. John Mnyika.
Nimemtumia ujumbe Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe
kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji
katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo
aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.
Aidha, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka
zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo
kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo ya maji kujirudia rudia
katika Jiji la Dar Es Salaam.
Pia, wajieleze kwa umma ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais
awachukulie kwa uzembe, kuisababishia hasara Serikali, kuathiri uchumi
wa nchi na maisha ya wananchi kwa kukosa maji mara kwa mara ambayo ni
huduma ya msingi ya binadamu na malighafi muhimu katika uzalishaji.
Itakumbukwa kwamba tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja
binafsi bungeni juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji
katika jiji la Dar Es Salaam, nikipendekeza Bunge kuingilia kati kuweza
kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka.
Iwapo hoja hiyo ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa
matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam mpaka hatua ya sasa
yangekuwa yamepungua katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo
nilipendekeza zichukuliwe.
Hata hivyo, badala ya kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingeisaidia
Wizara yake na kurekebisha udhaifu uliokuwepo na hivyo kumrejeshea
imani kwa umma ambavyo ilikuwa imepungua; Waziri Maghembe akaamua
kinyume cha kanuni za Bunge kutoa hoja ya kuondoa hoja niliyowasilisha.
Katika hatua hiyo nilijaribu kutumia kanuni za Bunge kuweza
kutoa ufafanuzi juu ya uongo wa Waziri Prof. Maghembe na hatua ambazo
Bunge lilipaswa kuchukua. Hata hivyo Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai
aliamua kukiuka kanuni kumlinda hali ambayo ilichochea vurugu bungeni.
Mara baada ya kurejea bungeni tarehe 10 Februari 2013
nilihutubia wananchi na kuwaeleza kusudio la kuandaa maaandamano kwenda
Wizara ya Maji iwapo katika kipindi cha ndani ya wiki mbili Waziri Prof.
Maghembe asingejitokeza kutoa maelezo kwa umma kuhusu masuala yote
ambayo alipaswa kuyajibu bungeni juu ya hatua za haraka zilizopaswa
kuchukuliwa.
Ndani ya wiki hizo mbili Waziri Maghembe alijitokeza mara mbili
kuzungumzia masuala ya maji Dar Es Salaam; kupitia mikutano ya CCM
ikiwemo katika kata ya Goba jimboni Ubungo na katika mkutano wake na
wafanyakazi DAWASA na DAWASCO tarehe 21 Februari 2013 na kueleza hatua
za haraka ambazo angesimamia zichukuliwe.
Hata hivyo, baada ya wiki moja bila ya Waziri wa Maji na Wizara
kwa ujumla kuonyesha kwa matendo kuisimamia kwa karibu EWURA, DAWASA,
DAWASCO na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka ambazo
nilizieleza kwenye hoja binafsi, niliamua kuchukua hatua zaidi.
Nilitangaza kuongoza maandamano ya wananchi tarehe 16 Machi 2013
kwenda Wizara ya Maji ili kupata majibu na kuisimamia Serikali kuchukua
hatua za haraka. Hata hivyo maandamano hayo yalizuiliwa na Jeshi la
Polisi kwa sababu zisizo za msingi na kuombwa kukata rufaa kwa Waziri wa
Mambo ya Ndani.
Nilikata rufaa lakini toka wakati huo mpaka anaondelewa katika
nafasi yake Waziri Dr Emmanuel Nchimbi alikwepa kuchukua hatua dhidi ya
aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela kwa
kuvunja sheria, kusababisha hasara na kuwanyima haki ya msingi wananchi
ya kufikisha ujumbe kwa Serikali.
Maandamano hayo yangefanyika na hatua kuchukuliwa matatizo
yangepungua tofauti na ilivyo sasa, hivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
Pereira Silima anapaswa kueleza umma lini rufaa hiyo itashughulikiwa
maandamano yaweze kufanyika wananchi wapate majibu ya hatua za haraka
nilizopendekeza ndani na nje ya Bunge.
Zaidi ya nusu mwaka umepita toka Waziri Prof. Maghembe atoe
ahadi ambazo ameshindwa kusimamia utekelezaji wake na hivyo kupaswa
kujiuzulu. Iwapo Waziri Prof. Maghembe hatajiuzulu nitaeleza hatua zaidi
ambazo nitachukua.
Wakati hatua hizo zikisubiriwa, natoa mwito kwa DAWASA na
DAWASCO kuhakikisha kwamba katika kipindi kisichozidi wiki moja huduma
za maji zinarejea katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata mgawo wa maji.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
10/01/2013
0 comments:
Post a Comment