KIGOGO WA MAGARI YA WIZI ANAKAMATWA....ADAIWA NDIYE MMILIKI WA KIWANDA CHA KUBADILISHIA MAGALI YA WIZI

Jengo ambalo linadaiwa ndiyo kiwanda hatari cha kubadilisha magari ya wizi, kimefumuliwa na mmiliki wake sasa hivi yupo nyuma ya nondo akingoja kufikishwa mahakamani.
Benovilla Luhanga, 43, ametajwa kuwa ndiye mmiliki wa kiwanda hicho na siku ananaswa, alikutwa na magari ya kihafari matano ambayo yote inadaiwa ni ya wizi.
Vilevile, Luhanga alikutwa na Bajaj moja ambayo imedaiwa nayo ni ya wizi na kwamba alikuwa tayari ameshaibadili rangi.
Luhanga alikamatwa akiwa na mkewe ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Kigogo huyo na mkewe, wanaishi ndani ya nyumba hiyo iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, kwa nje huonekana kama gereji lakini ndani ni makazi ya watu na shughuli za ubadilishaji magari, Bajaj na pikipiki hufanyika humo.
Luhanga na mkewe walikamatwa baada ya polisi kuvamia kiwanda hicho, saa 5 asubuhi lakini mchakato wa ukamataji ulikamilika saa 10 alasiri.
Mchakato wa kuwakamata uliwagharimu polisi jumla ya saa 5 kukamilika kwa sababu ilibidi kufanya upekuzi wa hali ya juu kwenye kiwanda hicho ili kubeba kila kitu kilichoonekana ni cha wizi.
Magari yote yaliyokutwa kwenye kiwanda hicho pamoja na Bajaj moja, ilidaiwa ni mali za wizi huku tayari yakiwa yameshabadilishwa rangi na kufungwa namba feki za usajili, isipokuwa gari moja.
ZA MWIZI ZILIVYOTIMIA
Habari zinaeleza kuwa kuwa kiwanda hicho kiligundulika kutokana na kijana mmoja ambaye aliwahi kuibiwa gari aina ya Toyota Canter, Goba, Dar, hivi karibuni.
Imebainika kuwa kijana huyo baada ya kuporwa gari hilo ambalo yeye alikuwa ameajiriwa kama dereva, maisha yalimwendea kombo kabla ya kwenda kwa Luhanga kuomba kazi, akidhani ni gereji.
Chanzo chetu kilitamka kuwa akiwa ndani ya kiwanda hicho, kijana huyo aliliona hilo Toyota Canter ndani ya uzio wa kiwanda hicho, hivyo kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kawe, Kinondoni, Dar.
“Baada ya kuripoti, askari walifuatilia na kukuta kweli kuna gari aliloibiwa kijana huyo na walipofanya upekuzi wakayakuta magari mengine matano yaliyoripotiwa kuibwa,” kilisema chanzo hicho.
Habari zinasema, polisi waliweza kubaini kuwa magari hayo baadhi yake yalibadilishwa rangi na kupakwa nyeusi huku namba za usajili nazo zikiwa zimebadilishwa.
KAMATAKAMATA IKAANZA
Polisi baada ya kugundua wizi huo, kamanda aliyeendesha oparesheni hiyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja, aliamuru Luhanga na mkewe wakamatwe na magari yaliyokuwa na uwezo wa kutembea yaliendeshwa, mengine yalikokotwa kwa ‘breakdown’ hadi Kituo cha Polisi Kawe.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa watuhumiwa hao tayari wamefunguliwa jalada katika kituo hicho kwa namba KW/RB/8194/2013 WIZI WA MAGARI.
Waandishi wetu walipofika kituoni Kawe Jumapili iliyopita, walikuta ndugu sita wa Luhanga wakihaha kutaka kuwawekea dhamana.

MAGARI YALIYOIBWA
Magari yaliyoibwa ni aina ya Nissan Navara lenye thamani ya shilingi milioni 45, lililokutwa na kibao cha usajili namba T519 BNP.
Lingine ni Toyota Harrier, ambalo thamani yake ni shilingi milioni 30. Hili lilikutwa na namba za usajili T 924 AXB, wakati kuna Toyota Rav4 new model, lenye thamani ya shilingi milioni 40 ambalo lilikutwa na namba T 581 BBL.
Gari lingine ni Toyota Canter, vilevile kulikuwa na Rav4 new model nyingine lenye rangi ya kijivu, hili lilikuwa limeng’olewa namba zake halisi bila kuwekewa nyingine.
Rav4 hilo ambayo halikufungwa namba, imeelezwa lilikuwa halijabadilishwa rangi, kwani kwa kawaida yale yanayoporwa na kuingizwa kiwandani humo, hupakwa rangi nyeusi.
OFISINI KWA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, ACP Camillius Wambura, hakuweza kupatikana licha ya waandishi kufika ofisini kwake. Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi wa jeshi hilo, alithibitisha kutokea kwa tukio.
“Tukio hilo lipo na tunaendelea na uchunguzi,” alisema ofisa huyo huku akiomba asiandikwe jina lake gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo.


0 comments:

Post a Comment

 
Design by Jambo Tz