LICHA ya biashara ya nyama ya nguruwe kupigwa marufuku kufuatia mlipuko wa homa ya nguruwe, bado inaendelea kufanywa kwa usiri mkubwa mjini Sumbawanga mkoani hapa. Mapema mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga iliweka chini ya karantini maeneo yote ya tarafa tano kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo mjini Sumbawanga na kupiga marufuku biashara hiyo, maarufu kama kitimoto.
Tarafa zilizowekwa chini ya karantini ni
Laela, Mwimbi, Matai, Mpui na Kasanga katika mwambao wa Ziwa
Tanganyika. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni, umebaini
biashara ya nyama hiyo ya nguruwe sasa inafanyika kwa usiri mkubwa
katika kitongoji cha Chanji mjini hapa, ambapo imebatizwa majina mapya
yakiwemo ‘mchicha, vodafasta na zunguka’.
Imebainika kuwa ni shida kwa mtu ambaye
hafahamiki na wauzaji wa nyama hiyo kuhudumiwa, kwa hofu ya kubambwa na
maofisa afya, hivyo ili uweze kuhudumiwa bila kutiliwa shaka lazima
unapoulizwa na mhudumu nini akuhudumie, lazima utamke majina hayo matatu
ya ‘zunguka vodafasta au mchicha’. Vingine huwezi kuhudumiwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa kitimoto
walikiri kupata faida kubwa, licha ya kwamba wanaifanya usiku kwa
kuogopa kukamatwa na maofisa afya kama wataifanya mchana.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi
kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini, walikiri kuwa licha ya
biashara hiyo kufanyika kwa usiri mkubwa tena usiku, bado nyama hiyo
huisha haraka, kwani walaji wake huigombania na kuinunua kwa wingi.
“Kabla ya karantini, nilikuwa nachinja
nguruwe mmoja mwenye uzito wa kilo 70, lakini nilikuwa nauza kwa shida
sana, baadae ilikuwa inalala, lakini cha ajabu licha ya marufuku
iliyowekwa, nachinja nguruwe watatu wenye uzito kati ya kilo 80 na 100
na inaisha mapema tu”, anasema.
Alisema “Tunauza kwa bei ile ile ya
awali ya Shilingi 2,500 kwa kilo, lakini bado faida ni kubwa mno kwani
inaisha yote, hata kama utakuwa na nyama yenye uzito wa kilo 1,000 au
tani moja, lazima itaisha tu, kasi ya walaji kwa sasa ni ya kutisha
kuliko ilivyokuwa kabla ya marufuku kuwekwa”.
Baadhi ya walaji wa nyama hiyo ya
nguruwe waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi katika kibanda kimoja
kinapouzwa, walikiri kuwa licha ya biashara hiyo kufanyika kwa usiri
mkubwa, tena usiku, bado wanainunua kwa bei ile ile ya awali.
“Ndugu yangu kumbe kitu chochote
kinachofanyika kwa usiri mkubwa ni kitamu, ebu shuhudia hapa jinsi watu
wanavyokula hii nyama kwa wingi, wengine wanafungasha na kupeleka
nyumbani wakihofia kukamatwa na maofisa wa afya. Hakika hii nyama sasa
imepata umaarufu wa kipekee licha ya kuwepo marufuku “, alisema John
Aswile, aliyetamba kuwa mlaji maarufu wa nyama hiyo.
Akifafanua, alisema kuanzia saa moja
usiku ukifika katika kibanda hicho, utakuta tayari nyama imeshakaangwa
na kufungwa katika vifurushi vya kuanzia kilo moja hadi tatu.
Alisema neno ‘zunguka’ linamaanisha kuwa
unakula papo hapo, hivyo unazunguka na kukaa mahali palipotayarishwa
rasmi. Alisema mteja anapomweleza mhudumu kuwa anataka ‘vodafasta’ moja,
anapewa kifurushi cha kilo moja na kuondoka nacho baada ya kulipia.
Akisema anataka ‘mchicha’ anapewa
kifurushi cha nyama hiyo, kilichokaangwa pamoja na mchicha. Karantini
hiyo ilitangazwa mapema mwaka huu na Daktari wa Mifugo na Mkaguzi wa
Mifugo, Dk Seleman Kataga.
Alionya kwamba kuanzia sasa, hakuna
ruhusa ya kuondoa kuingiza, kupitisha au kuchinja mifugo katika maeneo
yaliyo chini ya karantini. Vilevile alipiga marufuku usafirishaji wa
nguruwe kutoka kijiji kimoja hadi kingine ndani na nje ya maeneo hayo.
Alisema “Biashara yoyote ya nguruwe na
mazao yake, ikiwemo nyama, mbolea, manyoya, mifupa, ngozi na vyakula vya
kusindikwa, imepigwa marufuku iwapo itafanyika bila idhini ya kibali
cha maandishi cha daktari mwenye dhamana .“
Katika tarafa hizo zilizokumbwa na
mlipuko wa homa hiyo, tayari nguruwe 4,181 wamekufa. Kabla ya ugonjwa
huo, kulikuwa na nguruwe 28,630 na sasa wamebaki 24,449.
Ugonjwa huo uliingia wilayani humo kwa
mara ya kwanza mwezi Julai 2011 kupitia nguruwe hai, walioingizwa
kijijini Chombe Kata ya Kaoze Kata ya Chilulumo Wilaya ya Mbozi mkoani
Mbeya.
0 comments:
Post a Comment